SERIKALI imemtaka Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk. Tulia Ackson, kutumia nafasi hiyo kuhakikisha analinda maslahi ya Tanzania katika jumuiya za kimataifa.
Maagizo hayo yametolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, leo tarehe 30 Oktoba 2023, katika hafla ya kumpokea Dk. Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania, iliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri Majaliwa amesema, Serikali ina mikataba mingi iliyoingia katika Umoja wa Mataifa, hivyo inaamini Spika Tulia atatumia nafasi hiyo kupenyeza ajenda za Tanzania.
“Sisi tumefarijika kama Serikali, sababu moja kati ya majukumu yako kwamba utakuwa unahudhuria vikao vyote vya Umoja wa Mataifa na sote tunajua kwamba Serikali yetu tunayo mikataba yetu tuliyokuwa nayo kwenye Umoja wa mataifa,”
“ Sisi tunashukuru sababu tutakutumia utakapokuwa unaenda kwenye vikao kwa kuingiza ajenda za nchi. Tuna hakika utatupigania,” amesema Waziri Majaliwa.