Mchezaji wa zamani wa klabu ya Lile, Chelsea na Real Madrid, Eden Hazard ametangaza kustaafu kucheza soka akiwa na umri wa miaka 32.
Mbelgiji huyo hakuwa na kiwango bora tangu amejiunga na Real Madrid akitokea Chelsea 2019 kwa dau la Euro milioni 115 kutokana na kusumbuliwa na majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Hazard amestaafu akiwa amecheza jumla ya mechi 749 katika ngazi ya vilabu michuano yote na kufunga magoli 200 na usaidizi wa mabao mara 197 na makombe 15.
Hazard aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram:
“Lazima ujisikilize na kusema acha kwa wakati unaofaa. Baada ya miaka 16 na zaidi ya mechi 700 kucheza, nimeamua kukatisha maisha yangu kama mwanasoka wa kulipwa.
“Niliweza kutimiza ndoto yangu, nimecheza na kufurahia kwenye viwanja vingi ulimwenguni.
Wakati wa kazi yangu nilibahatika kukutana na wasimamizi wakuu, makocha na wachezaji wenzangu – asante kwa kila mtu kwa nyakati hizi nzuri, nitawakosa nyote.
“Shukrani za pekee kwa familia yangu, marafiki zangu, washauri wangu na watu ambao wamekuwa karibu nami katika nyakati nzuri na mbaya.
“Mwisho, asante sana, mashabiki wangu, ambao mmenifuata kwa miaka hii yote na kwa kunitia moyo kila mahali nilipocheza.
“Sasa ni wakati wa kufurahia wapendwa wangu na kuwa na uzoefu mpya. Tuonane nje ya uwanja hivi karibuni marafiki zangu.”
Kila jema kwako Eden Hazard