Naibu Waziri Uchukuzi, David Kihenzile ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kupeleka taa za kuongoza ndege katika maeneo ambayo yanatajwa kuwa ni malango makuu ya utalii akiwekea mkazo Arusha na Iringa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam amesema Tanzania ni ya pili kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii duniani ambapo asilimia 80 ya watalii hupita Kaskazini, huku Arusha ikitumika kama lango, hivyo taa hizo ni muhimu kufungwa katika uwanja wa ndege Arusha.
Kwa upande mwingine, ameagiza kushughulikiwa kwa malalamiko ya mara kwa mara kuhusu mizigo ya abiria kuchanganywa na mingine kupotea na wakati mwingine kuwasumbua abiria kwenye ufuatiliaji wa mizigo yao na kuutaka uongozi wa mamlaka hiyo kuwabaini wanaosababisha changamoto hiyo na kuwachukulia hatua.
Aidha, Kihenzile ameielekeza mamlaka hiyo kushughulikia malalamiko kuhusu ucheleweshwaji wa abiria katika eneo wanalopita wageni mashuhuri unaosababishwa na utaratibu wa malipo uliowekwa eneo hilo unaosababisha foleni kutokana na mfumo wa malipo unaoelezwa kuwa sio rafiki.